Home... |... EANA... | ...English News... | ...Kiswahili News... | French | ....Archives. ... |... ..Audio.. | ... Photo Gallery
 

MAHAKAMA YA AFRIKA KUHAMASISHA WADAU MISRI NA TUNISIA KUHUSU HAKI ZA BINADAMU

Na Kulwa Mayombi, EANA

Arusha, 6 April, 2017 (EANA)--Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) yenye Makao yake makuu Jijini Arusha itafanya ziara za kikazi nchini Misri na Tunisia wiki ijayo ili kukutana kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali kwa lengo la kuitangaza Mahakama hiyo.

Katika ziara hizo zitakazofanyika kuanzia April 09 hadi 14 mwaka huu,wajumbe wake ambao ni pamoja na majaji watatu wa Mahakama hiyo na baadhi ya maafisa wa  ofisi ya msajili wa Mahakama, pia watakutana na Marais wa nchi hizo za Misri na Tunisia, mawaziri wa mambo ya kigeni,mawaziri wa sheria pamoja na maspika wa mabunge ya nchi hizo.

Rais wa Mahakama ya Afrika, Mheshimiwa Jaji Sylvian Ore’ ,amesema wakati wa ziara hiyo itaendeshwa semina inayolenga kukuza uelewa wa wadau hao juu ya uwepo wa Mahakama hiyo.

AfCHPR
 
 
 
 
 
 

Kwa mujibu wa Jaji Ore’, uelewa wa wadau hao kuhusu uwepo wa Mahakama ya Afrika pia utaleta hamasa kwa nchi nyingi zaidi za Umoja wa Afrika(AU) kuridhia itifaki iliyoanzisha Mahakama hiyo na kutoa tamko rasmi la kutambua na kukubali mamlaka ya Mahakama hiyo kuweza kupokea kesi za watu binafsi na Mashirika yasiyo ya kiserikali(NGO’s).

“Ili Mahakama iweze kufanikisha malengo yake na pia kuimarisha mfumo wa haki za Binadamu barani Afrika,nchi nyingi za umoja wa Afrika  hazina budi kuridhia itifaki iliyounda Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu kwa mujibu wa kifungu cha 34(6)”, alisema Rais huyo wa AfCHPR.

Hadi Machi mwaka huu ni nchi saba tu kati ya nchi 30 zilizoridhia itifaki , ndio zimetoa tamko rasmi la kutambua na kukubali mamlaka ya mahakama  hiyo kuweza kupokea kesi za watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Nchi hizo saba ni pamoja na Benin,Burkina Faso Ivory Coast ,Ghana,Mali,Malawi naTanzania.
Tangu mwaka 2010,Mahakama hiyo ya Afrika  imefanikiwa kuendesha programu mbalimbali zinazolenga kutoa elimu ya uwepo wa Mahakama hiyo pamoja na shughuli zake katika baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Chad,Ethiopia,Afrika ya Kusini, Ghana, Malawi, Kenya, Uganda, Zambia na Ivory Coast.

Mahakama ya Afrika  ilianzishwa kwa mujibu wa kifungu namba 1 cha Itifaki ya mkataba ulioanzisha Mahakama hiyo ambapo Itifaki hiyo ilikubaliwa juni 09,1998 nchini Burkina Faso na ikaanza kutumika januari 25,2004 na ilianza shughuli zake rasmi Novemba 2006.

Aidha hadi Machi mwaka huu, jumla ya maombi 138 ya mashauri yali pokelewa na mahakama hiyo na kesi 32 zimekamilishwa.

Mwisho

 
Home...English News.. .Kiswahili News..French