Home... |... EANA... | ...English News... | ...Kiswahili News... | French | ....Archives. ... |... ..Audio.. | ... Photo Gallery
 

6MAHAKAMA YA AFRIKA : KUJITOA KWA RWANDA HAKUTAATHIRI KESI YA VICTOIRE INGABIRE

Na Balthazar Nduwayezu, EANA

Arusha, 6 Juni 2016 (EANA)—Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu iliyoko mjini Arusha nchini Tanzania, imeamua kuendelea kusikiliza kesi ya mwanasiasi aliifungwa Bi Victoire Ingabire Umuhoza dhidi ya serikali ya Rwanda, licha ya Rwanda kuamua kufuta Tamko la kukubalia raia wake kupeleka mashauri kwenye Mahakama hiyo.

Katika hukumu iliyosomwa Mahakamani hapo juzi na jaji El Haj Guissé kutoka Senegal kwa niaba ya wenzake, Mahakama inaeleza kuwa serikali ya Rwanda imechukua uamuzi wa kufuta Tamko baada ya muda mrefu wakati shauri la Bi Ingabire ilikuwa imeshawasili mahakamani hapo.

« Mahakama, kwa wingi wa majaji tisa dhidi ya wawili, jaji Agusito Ramadhani(Tanzania) na Gerard Niyungeko (Burundi) wakiwa wametoa maoni tofauti, inaona kitendo cha Mlalamikiwa kuondoa Tamko alilofanya kuafuatia kifungu 44 (6) cha sheria ya Mahakama, kimekuja miezi kumi na mbili baada ya shauri kuwasilishwa(…). Kwa pamoja, Mahakama imeamua kuwa kuondoa tamko hilo hakuathiri hata kidogo shauri la mlalamikaji, hivyo Mahakama ina mamlaka ya kuendelea kulisikiliza» ameeleza Jaji Guissé.

Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu
 
 
 
 
 
 

Kwenye Itifaki ya kuunda Mahakama hiyo, sheria inataka nchi wanachama walioridhia Itifaki hiyo, kutoa Tamko la kuruhusu watu binafsi na Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kuleta kesi moja kwa moja kwenye Mahakama hiyo, lasivyo Mahakama haina mamlaka ya kuwasikiliza.

Madame Ingabire aliwasilisha shauri lake tarehe 30 Octoba 2014. Mahakama ililipokea maana vigezo vyote vilikuwa vimezingatiwa.

Lakini tarehe 1 Machi 2016, siku tatu kabla ya kesi yake kuanza kusikilizwa, serikali ya Rwanda iliamua kufuta Tamko lake, na hivyo kudai kuwa kesi hiyo haina budi kutupiliwa mbali.

Mahakama iliagiza pande mbili, yaani serikali ya Rwanda na utetezi wa Ingabire kuleta hoja zao juu ya aidha kesi kusimama na kufutwa au kuendelea.
Ni baada ya kupitia hoja za pande mbili, ambapo Mahakama imeamuru kesi kuendelea. Hata hivyo tarehe ya kuendelea kwa kesi haikutajwa.
Katika kesi hiyo, Bi Ingabire anatetewa na wakili Gatera Gashabana kutoka Rwanda na Dr Caroline Buisman kutoka Uholanzi, wakati serikali inawakilishwa na Rubango Epimaque kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu nchini mwake.

Bi Ingabire , anayetumikia kifungu cha miaka 15 nchini Rwanda, analalamikia serikali ya Rwanda kukiuka haki zake za msingi wakati wa kukamatwa kwake na kusikilizwa kwa kesi yake kwenye mahakama za Rwanda.

Bi Ingabire Victoire Umuhoza(48) alikuwa nchini Uholanzi akifanya masomo yake ya elimu ya juu ya Uchumi na Biashara wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994 . Mwaka 2000 aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama RDR kilichokuwa kikifanyia shughuli zake uhamishoni. Baadaye aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Muungano wa chama hicho na chama cha FRD, uliojulikana kwa jina na FDU.

Mwaka 2010, baada ya miaka 17 nje ya nchi, aliamua kurudi Rwanda, kusajili chama kipya hicho, na baadaye kugombea urais, kupambana na jenerali Paul Kagame.

Mama huyo lakini hakufikia ndoto zake, maana mapema Februari 2010 alianza kusumbuliwa na polisi, na baadae Aprili 23, 2010 kutiwa mbaroni na kushitakiwa kwa makosa mbali mbali ikiwa ni pamoja na kueneza fikra za mauaji ya kimbari, kuhatarisha usalama wa nchi, na kushirikiana na makundi ya kigaidi.

Alihukumiwa kifungo cha miaka minane jela na Mahakama kuu, na baadae miaka 15 na mahakama ya juu.

Uamuzi wa Mahakama ya Afrika ya kuendelea kusikiliza kesi yake licha ya Rwanda kufuta Tamko, inayapa njia mashauri ya Wanyarwanda wengine yaliyowasilishwa mwaka 2015, ikiwa ni pamoja na Kayumba Nyamwasa, Kennedy Gihana na wengine, Rutabigwa Chrisanthe na Laurent Munyandilikirwa.

BN/LC/MM/NI

 
Home...English News.. .Kiswahili News..French