Home... |... EANA... | ...English News... | ...Kiswahili News... | French | ....Archives. ... |... ..Audio.. | ... Photo Gallery
 

CHAD KURIDHIA ITIFAKI ILIYOANZISHA MAHAKAMA YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU

Na Kulwa Mayombi, EANA

Arusha, 24 December, 2015 (EANA)--Rais wa Chad Idriss Deby amesema nchi yake itaridhia itifaki iliyoanzisha Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) na kutoa tamko la kuruhusu watu binafsi na mashirika ya watu binafsi (NGOs) kupeleka kesi moja kwa moja mbele ya Mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini Arusha, Tanzania.

Rais huyo wa Chad ameyasema hayo mwishoni mwa wiki alipompokea Rais wa Mahakama hiyo Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania Augustino Ramadhani katika ikulu ya nchi hiyo.

Rais Deby alipongeza kazi zinazofanywa na mahakama hiyo na na kuongeza kuwa nchi yake imepata hamasa ya kuridhia itifaki iliyounda mahakama hiyo ya Afrika ya haki za binadamu na watu na kuruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kupeleka kesi zao moja kwa moja mbele ya mahakama hiyo.

Jaji Ramadhani
 
 
 
 
 
 

Chad itatakuwa nchi ya 30 ya Afrika kuridhia na ya nane kutoa tamko kuruhusu NGOs na watu binafsi kupeleka kesi.

Jaji Ramadhani alimshukuru Rais huyo wa Chad kwa uhakikisho aliioutoa wa kuridhia itifaki hiyo pamoja na tamko lake.

Aidha aliishukuru serikali hiyo ya Chad kuwa mwenyeji wa semina 15-16 Decemba iliyoshirikisha wajumbe zaidi ya 100 wakiwemo viongozi wa serikali, wizara husika, vyama vya wanasheria, wanaharakati na kamisheni za haki za binadamu kutoka nchi za Chad, Gabon, Cameroon, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Semina hiyo ilitanguliwa na mafunzo ya siku moja kwa vyombo mbalimbali vya habari na wahariri iliyofanyika tarehe 14 Desemba.

Kuanzia 2010 hadi sasa Mahakama hiyo ya Afrika imeendesha programu mbalimbali zenye lengo la kuitambulisha mahakama hiyo na tayari ziara 24, semina na mikutano 9 ya kikanda yenye lengo hilo la kuitambulisha mahakama imeshafanyika.

Lengo kuu la ziara hizo za uelemishaji ni kukuza na kulinda haki za binadamu barani Afrika ambapo lengo mahususi linajumuisha kukuza uelewa wa wananchi kuhusu Mahakama hiyo, kuzihamasisha Nchi za Afrika kuridhia na kutoa tamko kwa mujibu wa kifungu 34 (6) cha itifaki ya kukubali kuruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) kuleta kesi moja kwa moja mbele ya mahakama hiyo.

Tangu kukubaliwa kwa itifaki ya kuanzisha mahakama hiyo ya Afrika mwaka 1998, ni nchi 29 tu kati ya 54 wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) ndizo zilizoridhia itifaki hiyo.

Nchi zilizoridhia itifaki kufikia Desemba 2015 ni :Algeria, Benin, Burkina Faso, Burundi, Cameroon, Cote d'ivoire, Comoros, Congo, Gabon, The Gambia, Ghana, Kenya, Libya, Lesotho, Malawi, Mali, Mauritania, Mauritius, Msumbiji, Nigeria, Niger, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya kidemokrasia ya Sahrawi , Senegal,Afrika ya Kusini, Tanzania, Togo na Tunisia.

Aidha kati ya nchi hizo 29 zilizoridhia itifaki nii nchi 7 tu ndizo zilizotoa tamko la kukubali mamlaka ya mahakama kuweza kupokea kesi za watu binafsi na NGOs. Nchi hizo ni Burkina faso, Ivory coast, Ghana, Malawi, Mali, Rwanda na Tanzania.

KM/LC/MM/NI

 
Home...English News.. .Kiswahili News..French