Home... |... EANA... | ...English News... | ...Kiswahili News... | French | ....Archives. ... |... ..Audio.. | ... Photo Gallery
 

MAHAKAMA YA AFRIKA YATAKA WANACHAMA WA AU KUHARAKISHA KURIDIHIA ITIFAKI

Na Kulwa Mayombi, EANA

Arusha, 21 Desemba, 2015 (EANA)--Mahakama ya haki za binadamu na watu (AfCHPR) imetoa wito kwa Nchi wanachama wa Umoja Wa Afrika ( AU) kuharakisha kuridhiwa kwa itifaki iliyoanzisha mahakama hiyo na kutoa tamko la kukubali mahakama kuweza kupokea kesi za watu binafsi na taasisi zisizo za kiserikali ( NGOs) .

Rais wa mahakama hiyo yenye makao yake makuu Mjini Arusha Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania Augustino Ramadhani alisema kwa kufanya hivyo mahakama hiyo itakuwa na mamlaka ya kushughulikia kazi zake kikamilifu.

“Ukamilifu wa mahakama hiyo ya haki za binadamu na watu unahitaji uungwaji mkono na wadau wote hasa kutoka Nchi 54 wanachama wa umoja wa Afrika” alisisitiza Jaji Ramadhani wakati anahutubia wajumbe kutoka ukanda wa Afrika ya kati katika semina iliyofanyika Ndjamena Nchini Chad mwishoni mwa wiki. Semina hiyo ililenga kutoa elimu kwa wadau hao kuhusu umuhimu wa mahakama hiyo.

Hadi sasa ni Nchi 7 tu kati ya 29 ndizo zilizoridhia itifaki na kutoa tamko la kukubali mamlaka ya mahakama kuweza kupokea kesi za watu binafsi na NGOs kwa mujibu wa kifungu 34(6) cha itifaki ya kukubali kuruhusu watu binafsi na NGOs kuleta kesi moja kwa moja mbele ya mahakama hiyo. Itifaki husika ilisainiwa na viongozi wa Afrika miaka 16 iliyopita. Kwa mujibu Jaji Ramadhani baadhi ya nchi wanachama hadi sasa hazijaridhia na kutoa tamko kuhusu itifaki hiyo tangu kukubaliwa kwa itifaki hiyo mwezi juni 1998 Nchini Burkina Faso.

Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania Augustino Ramadhani
 
 
 
 
 
 

Akifungua Semina hiyo waziri mkuu wa Chad,Kalzeubet Pahimi alisema haki za binadamu ni kitovu cha heshima na utu wa mwafrika. Alielezea matarajio yake kuwa semina hiyo itawaongezea uelewa zaidi wajumbe kuhusu kazi za mahakama hiyo na umuhimu wake na kusisitiza kuwa nchi yake itaharakisha kuridhia itifaki iliyoanzisha mahakama hiyo na kuhimiza nchi zingine za ukanda wa afrika ya kati ambazo hazijaridhia itifaki kufanya hivyo haraka.

“Mahakama hiyo ya haki za binadamu na watu ipo kwa ajili ya kulinda haki za binadamu na hivyo ni lazima tuwe mstari wa mbele kuiunga mkono” aliwaambia wajumbe zaidi ya 100 wakiwemo maafisa wa serikali, wizara husika, vyama vya sheria na kamisheni za haki za binadamu kutoka Chad, Gabon, Cameroon, Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo(DRC) pamoja na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kwa upande wake chama cha wanasheria cha nchini Chad kilisema semina hiyo imeendeshwa wakati muafaka ambapo nchi hiyo inafanya maboresho katika mfumo wake wa masuala ya sheria.

Semina hiyo ilitanguliwa na mafunzo ya siku moja kwa vyombo mbalimbali vya habari kutoka ukanda wa Afrika ya kati ambapo Jaji Ramadhani alisisitiza jukumu kubwa la vyombo vya habari kuwa ni pamoja na kukuza masuala ya haki za binadamu barani Afrika.

“Usambazaji wa habari zinazohusu mahakama ya Afrika kutasaidia kukuza masuala ya haki za binadamu na pia kusaidia kuweka msingi imara wa kuwa na jamii inayoishi katika misingi ya demokrasia katika nchi zetu ambazo zimekuwa ni wahanga wa ukoloni, umasikini na maendeleo duni” Jaji Ramadhani aliwaambia waandishi hao na wahariri.

Kuanzia Desemba 2010 hadi sasa Mahakama hiyo ya Afrika ya Haki za Binadamu na watu imeendesha programu mbalimbali zenye lengo la kuitambulisha mahakama hiyo na tayari ziara 24, semina na mikutano 9 ya kikanda yenye lengo hilo la kuitambulisha mahakama imeshafanyika.

Lengo kuu la ziara hizo za uelemishaji ni kukuza na kulinda haki za binadamu barani Afrika ambapo lengo mahususi linajumuisha kukuza uelewa wa wananchi kuhusu Mahakama hiyo, kuzihamasisha Nchi za Afrika kuridhia na kutoa tamko kwa mujibu wa kifungu 34 (6) cha itifaki ya kukubali kuruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya serikali (NGOs) kuleta kesi moja kwa moja mbele ya mahakama hiyo.

KM/LC/MM/NI

 
Home...English News.. .Kiswahili News..French