Home... |... EANA... | ...English News... | ...Kiswahili News... | French | ....Archives. ... |... ..Audio.. | ... Photo Gallery
 

WAKENYA YA MAUAJI NA UNYANG’ANYI KUSIKILIZWA ARUSHA

Na Mtua Salira, EANA

Arusha, Mei 17, 2015 (EANA) — Kesi ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha inayowakabili raia wa Kenya waliotiwa mbaroni Msumbiji na kuhamishiwa Tanzania miaka tisa iliyopita itasikilizwa na Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) Arusha Mei, 21, 2015.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mahakama hiyo, kesi hiyo ya Wakenya ijulikanayo kama Onyango na wenzake tisa, wanadaiwa kutenda makosa hayo mjini Moshi nchini Tanzania, itasikilizwa kwa siku moja.

Wakenya hao wanadai katika maombi yao kwamba walikuwa nchini Msumbiji katika shughuli zao kihalali kutafuta fursa za biashara lakini walitekwa kinyume cha sheria na kuingizwa kwenye ndege ya kijeshi na kurejeshwa nchini Tanzania Januari 16, 2006 kisha kushitakiwa kwa mauaji na mashitaka mengine matatu ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

AfCHPR
 
 
 
 
 
 

Mahakama hiyo ya Afrika pia itasikiliza maombi ya mtanzania Mohamed Abubakari, anayepinga adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa mashitaka mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha na Mahakama ya Wilaya ya Moshi Julai 1998. Maombi hayo yatasikilizwa Mei 22,2015.

Kesi hizo zitasikilizwa hadharani katika Ukumbi wa Kibo, makao makuu ya AfHCPR yaliyopo kwenye jengo la ofisi za Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), eneo la Burka, barabara ya Dodoma, mjini Arusha.

Nakala ya taarifa hiyo iliyotolewa kwa Shirika Huru la Habari la Afrika Mashariki (EANA) pia ilieleza kwamba Mahakama hiyo itafanya Kikao chake cha 37 cha Kawaida kuanzia Mei 18 hadi Juni 5, mwaka huu katika makao yake makuu.

Majaji wa Mahakama hiyo pamoja na mambo mengine watajadili na kupitisha Ripoti ya Mhula wa Kati wa Kazi za Mahakama kwa ajili ya kuwasilishwa kwenye Kikao cha 25 cha Wakuu wa Umoja wa Afrika (AU) kitakachofanyika Juni, Afrika Kusini na kuchambua maombi yaliyokwishawasilishwa mbele ya Mahakama hiyo.

Kikao hicho cha majaji kitatanguliwa na majaribio ya mafunzo kwa wahariri 20 waandamizi na waandishi wa habari wa Afrika Mashariki juu ya jukumu la vyombo vya habari katika kuhamasiha shughuli za Mahakama hiyo.

Mafunzo hayo yameandaliwa kwa ushrikiano kati ya AfHCPR na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ). Waandishi hao baadaye wataandika habari hizo mbili zitakazosikilizwa na mahakama hiyo wiki ijayo.

MS/LC/NI

 
Home...English News.. .Kiswahili News..French